Monday, 13 October 2014


Mwanafunzi wa shule ya msingi jijini Dar es Salaam mwenye umri wa miaka saba, ameuawa kikatili baada ya kubakwa, kuchinjwa na kunyofolewa sehemu zake za siri.

Mwanafunzi huyo wa darasa la kwanza (jina linahifadhiwa), mwili wake ulikutwa umetupwa kwenye shamba karibu na nyumbani kwao jana maeneo ya Mbezi Temboni, kata ya Saranga.

Akisimulia tukio hilo, mama wa mtoto huyo (jina linahifadhiwa), alisema kuwa juzi baada ya mwanawe kurejea toka shuleni alimuogesha na kumpa chakula majira ya saa 12 ya jioni.

Alisema baada ya kumtayarishia chakula hicho, alitoka kidogo kuelekea Temboni na aliporejea nyumbani  hakumkuta mtoto wake na ndipo alipokwenda kwa majirani kumtafuta.

Alisema mpaka saa 1 usiku hawakufanikiwa kumuona mtoto huyo licha ya kuambiwa mara ya mwisho alionekani akiwa anacheza na mtoto wa jirani yake.

Hata hivyo, alisema alipokwenda kwa jirani kumuulizia kama wamemuona, alijibiwa kuwa alionekana akiwa anacheza pembeni ya banda la nguruwe.

Alisema baada ya kufanya jitihada zote bila mafanikio aliamua kwenda kutoa taarifa  kituo cha polisi.

Aliendelea kusimulia kuwa jana majira ya saa 2 asubuhi, alipata taarifa ya kuonekana kwa mwili wa mtoto wake kwenye shamba moja  lililopo karibu na nyumbani kwake.

Alisema mwili wa mwanawe umekutwa ukiwa umepandishwa nguo alizovaa juu huku nguo ya ndani ikiwa imevuliwa.

Aidha, sehemu zake za siri zilikutwa zikiwa na uwazi kitendo kinachoonyesha kuwa aliingizwa kitu na kunyofolewa baadhi ya viungo.

“Roho inaniuma sana mwanangu jamani wamembaka na kisha kupanua sehemu zake za siri inaonyesha kuna vitu vimechukuliwa na shingo yake wamemkata hata kwenye kichwa chake karibu na paji la uso wamempiga kwa tofali,” alisema.

MMOJA WA WATUHUMIWA AKAMATWA
Baba wa mtoto huyo (jina linahifadhiwa) akizungumza huku akitokwa na machozi alisema mmoja kati ya watu waliofanya unyama huo amekamatwa.

"Pamoja na kukamatwa kwa mtuhumiwa lakini wameniachia kovu la huzuni," alisema.
Alisema mtuhumiwa huyo amewataja na wenzake wawili walioshiriki kufanya unyama huo ambao wanatafutwa na polisi.

Mwili wa mtoto huyo umehidhiwa katika Hospitali ya Tumbi na umeshafanyiwa uchunguzi.

Habari za uhakika ambazo NIPASHE imezipata ni kuwa mtuhumiwa aliyekamatwa alikutwa na damu kwenye chupi yake baada ya kukaguliwa na askari.

Mtuhumiwa huyo anayedaiwa kuonekana mara ya mwisho na marehemu, aliwataja wenzake baada ya kubanwa na askari.

MAJIRANI  WAZUNGUMZA
Akizungumza kwa niaba ya majirani, Halima Omary, alisema taarifa za kuonekana kwa mwili wa mtoto huyo walizipata kutoka kwa mmiliki wa shamba hilo baada ya kufika shambani kwake asubuhi na kuona kishimo cha damu.

Anasimulia kuwa baada ya kuona shimo hilo la damu alifuatilia michirizi ya damu hiyo shambani hapo ambayo ilikuwa ikionyesha kama kuna mtu kaburuzwa.

“Baada ya mama huyo kufuatilia damu hizo shambani kwake, ndipo alipokutana na maiti hiyo na kuondoka kwenda kutoa taarifa kwa majirani na watu walipofika wakagundua ni yule mtoto aliyekuwa akitafutwa baada ya kupotea,” alisema. 

Alisema baada ya kufika katika tukio hilo walimkuta mtoto huyo akiwa amejeruhiwa katika maeneo ya sehemu zake za siri, kifuani, shingoni na kichwani.

Omary alisema kuna haja ya serikali kuwachukulia hatua watu wenye mapori ambao hawayaendelezi ili yasitumike kufanyia matukio kama hayo.

Naye  Marry Machange ambaye ni jirani wa marehemu aliitaka  serikali iingilie  kati suala hilo, kwani katika Kata ya Saranga kuna mapori makubwa ambayo yanatakiwa kuendelezwa hata kwa kujengwa zahanati kuliko kuachwa kuwa sehemu za kufanyia mauwaji.

Mwenyekiti wa Serikali ya  Mtaa kata ya Saranga, Godwin Muro, alikiri kutokea kwa tukio hilo.

Alisema alipata taarifa za kupotea kwa mtoto huyo saa 12 jioni na kuamua kusambaza taarifa hiyo katika kituo cha polisi cha Mbezi na kwa wananchi.

Mjumbe wa nyumba 10 shina namba 25 katika eneo hilo, Asibwene Mwaipopo, alisema tukio hilo ni la kinyama na halijawahi kutokea katika eneo hilo.

Naye  Diwani wa kata ya Saranga, Efyemu Kinyafu, alisema amepokea taarifa hiyo kwa masikitiko makubwa na kuwataka wananchi wasubiri majibu kutoka kwa polisi ambao wanaufanyia uchunguzi mwili wa marehemu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa mtoto huyo katika maeneo ya shingoni amekatwa na kitu chenye ncha kali.

“Kuna tatizo limeonekana huenda ameingiliwa sana hivyo siwezi kuthibitisha kama sehemu zake zimekatwa kuna mambo mengine hayapaswi kuzungumzwa ni ya kidaktari zaidi,” alisema.

Kamanda Wambura alisema mpaka sasa wamefanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja na wengine wawili wanaendelea kuwasaka ili hatua za kisheria zichukuliwe.

0 comments:

Post a Comment

Design by GG greggy| Blogger Theme by greggy - Premium Blogger Templates | NewBloggerThemes.com