Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi.
Na Mwandishi wetu
MWINJILISTI wa Kanisa la Baptist, lililopo halmshauri ya Busokelo wilayani Rungwe, mkoani Mbeya, Ambumbulwisye Mwasomola (35), ameuawa kwa kupigwa na mchi kichwani na mtu aliyekuwa akimuombea.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo wanadai aliyekuwa akiombewa alikuwa na tatizo la akili.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, alisema tukio hilo limetokea Septemba 27, mwaka huu majira ya saa tano usiku
Msangi alisema tukio hilo lilitokea katika kijiji cha Lukasi, kata ya Lwangwa, tarafa ya Busokelo ambapo mtuhumiwa aliyehusika ni Swalapo Mwaisanila (56) ambaye ni mgonjwa wa akili
Alisema mtuhumiwa huyo alichukua mchi na kumpiga nao Mwinjilisti huyo wakati akijaribu kumuombea hali iliyosababisha kifo chake
Alisema baada ya tukio hilo polisi wamemkamata mtuhumiwa na taratibu mbalimbali zinaendelea ili kumfikisha katika vyombo kisheria
Katika tukio jingine mkazi wa Mwanavala wilayani Mbarali aliyefahamika kwa jina moja la Kabote ameuawa kwa kuchomwa mikuki sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kushindwa kulipa sh 500 alizokuwa akidai
Marehemu alikuwa akidaiwa kiasi hicho cha fedha na mmiliki wa kilabu cha pombe za kienyeji, Nyamaniengo Kinanga, baada ya kunywa pombe
Kamanda Msangi, alisema tukio hilo limetokea Septemba 28, tano usiku wakati marehemu akinywa pombe kwenye kilabu cha mtuhumiwa
Alibainisha kuwa baada ya marehemu kushindwa kulipa fedha hizo na mtuhumiwa aliamua kumchoma na mkuki
Kutokana na tukio hilo watu 13, wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano kwakuwa baada ya marehemu kushindwa kulipa fedha hiyo walianza kumkimbiza huku wakipiga kelele.
Msangi alisema msako unafanyika ili kuwakamata watuhumiwa wengine akiwemo waliokimbia mara baada ya tukio