Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela


Mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Iglansoni, ameuawa kwa kupigwa risasi kichwani kwa bahati mbaya na askari polisi waliokuwa katika jitihada za kumkamata mtuhumiwa wa ujambazi.

Aliyeuawa ni Joyce Maragabu (65), ambaye anadaiwa kupigwa risasi na askari hao waliokuwa wakijihami na kundi la watu waliotaka kuwavamia ili wasimkamate mhalifu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela, alisema askari hao walikuwa wanataka kumkamata, Nkida Gwisu, anayetuhumiwa kumshambulia mtu mwingine, lakini kwa bahati mbaya risasi hiyo ikampiga kichwani mwanamke huyo aliyekuwa anafua nguo nyumbani kwake.

Kamwela alisema, tukio hilo lilitokea juzi Oktoba 16, saa 6 mchana.

Alisema askari polisi wawili ambao hakuwataja majina yao wa kituo kidogo cha polisi Ihanja, walifika katika kitongoji hicho ili kutoa ulinzi mnadani, lakini baadaye walipewa taarifa kuhusu mtuhumiwa huyo kumshambulia mmoja wa wanakijiji.

Alisema wakati wakiwa katika jitihada ya kumtafuta mhalifu huyo, alitokea mwananchi mmoja aliyedai kumfahamu mtuhumiwa huyo, hali iliyorahisisha kazi ya kumkamata na kumweka chini ya ulinzi.

Hata hivyo, alisema baadaye mtuhumiwa huyo alianza vurugu, hali iliyosababisha kundi kubwa la watu kwenda eneo hilo wakiwa na silaha za jadi ikiwamo mawe, pinde, mishale, fimbo na mapanga, na kuanza kumshambulia mmoja wa askari polisi aliyemshikilia mhalifu huyo.

Alisema kuwa katika hali ya kutaka kumwokoa mwenzake, askari aliyekuwa na bunduki alifyatua risasi moja ya moto hewani, lakini hata hivyo wakiwa kwenye purukushani, ndipo risasi moja ilifyatuka na kumpiga kichwani mwanamke huyo.

Kamwela alisema baada ya tukio hilo, wananchi waliokuwa na hasira waliichoma moto pikipiki ya askari hao, yenye namba za usajili PT 3242 –Yamaha na kuiteketeza.

Alisema kutokana na vurugu hizo, askari hao walijeruhiwa vibaya baada ya kupigwa na kundi hilo na tayari jeshi hilo linawashikilia askari hao kwa mahojiano zaidi.