Wednesday, 3 September 2014


KUNRADHI KWA PICHA HIZI. MATUKIO HAYA YANAZUILIKA, KWANINI WATAWALA WANAPENDA KUMWAGA DAMU?
Tazama unyama wa Polisi!

Na Daniel Mbega
KICHWA cha habari kilichonivutia ni ‘Kova aongeza idadi ya ‘tume’ D’Salaam’ ambacho kipo kwenye gazeti la Mwananchi toleo la Jumatano, Septemba 3, 2014.
Habari hii imefuatia hatua iliyofanywa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, baada ya kutangaza jopo la wapelelezi kuchunguza kifo cha mtuhumiwa Liberatus Matemu (55) aliyefia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akidaiwa kupigwa na polisi katika Kituo cha Stakishari na maiti yake kukataliwa na nduguze. Kabla ya kufariki Jumapili iliyopita, Matemu alikuwa chini ya ulinzi katika kituo hicho kilichopo wilayani Ilala ambako alikaa kwa siku nane. Jopo hilo la wapelelezi litaongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Costantine Masawe.
Tumeshazowea kusikia ‘tume’ zikiundwa kila yanapotokea matukio mbalimbali, mengi yakiwa yamefanywa ama kuwahusisha hao hao wanaounda tume hizo. Mifano iko mingi, na inadhihirishwa na vichwa vya habari kama vile… “Jeshi la Polisi launda Tume kuchunguza mauaji ya Mwangosi!”, “Tume ya kuchunguza majuaji Morogoro yaundwa!”, “Walioua raia Songea wachunguzwa!”, “Polisi wachunguza mauaji Nyamongo!”, “Msako waanza utekwaji wa Kibanda!” “Aliyemteka Dk. Ulimboka hajulikani!” “Mabomu ya Arusha yaacha maswali”.
Naam, vichwa vya habari vya aina hii vimekuwa vikijitokeza kila wakati kwenye vyombo vya habari nchini kila mara yanapotokea mauaji katika vurugu mbalimbali, na mauaji haya mara nyingi yamekuwa yakisababishwa ama kufanywa na askari wa jeshi hilo hilo la polisi.
Lakini ukitazama jopo lililoundwa na Kamanda Kova, binafsi nasema ni usanii mwingine unaoendelea kwa sababu mpaka sasa hakuna taarifa zozote za uchunguzi zilizotolewa na kamanda huyo kuhusu matukio kadhaa yaliyotangulia, ambayo alidai yanachunguzwa baada ya kuyaundia ‘tume’.
Itakumbukwa kwamba, Julai 23, 2014, Kova huyo huyo aliunda timu ya wataalamu saba kuchunguza kashfa ya viungo vya binadamu vilivyookotwa Mbweni Mpiji, wilayani Kinondoni ambavyo vilidaiwa vilikuwa vikitumiwa katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Afya (Imtu) lakini hadi sasa wananchi hawajajulishwa kuhusu majibu ya uchunguzi huo.
Aidha, Mei 21, 2014, Kova aliunda tena jopo la wapelelezi liliongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jaffari Mohamed kuchunguza kifo cha aliyekuwa Meneja Biashara ya Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Julius Gashaza aliyedaiwa kujinyonga na hadi leo taarifa za uchunguzi huo hazijatangazwa.
Mnamo Januari 7, 2014, Kamanda Kova aliunda jopo la wapelelezi nane walioongozwa tena na RCO Jaffari Mohamed kuchunguza tukio la kutekwa Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Temeke, JosephYona na matokeo yake hayajawekwa wazi.
Wanahabari nchini Tanzania jana walikuwa wanakumbuka miaka miwili ya mauaji ya kinyama yaliyofanywa na askari wa jeshi la polisi dhidi ya mwandishi wa kituo cha Chennel Ten, marehemu Daudi Mwangosi, wakati polisi hao ‘wakipambana’ na wafuasi wa Chadema waliokuwa katika ufunguzi wa tawi la chama hicho katika Kijiji cha Nyololo mkoani Iringa.
Lakini kutekwa na kuteswa kwa Mhariri Mtendaji wa New Habari, Absalom Kibanda pamoja na kutekwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, bado kumeacha makovu mengi yasiyofutika.
Wakati katika matukio yote ya mauaji polisi ndio wanaohusika, bado jeshi hilo hilo linaibuka na kuunda tume ya kuwachunguza polisi wenzao walioua, hatua ambayo kwa ujumla inaleta mkanganyiko na ndiyo maana ninasema ni ‘Tume za Manyani kuchunguza nani kala mahindi’!
Hivi inakuwaje nyani amchunguze nyani aliyekula mahindi wakati huyo huyo anayemchunguza mwenzake kesho naye atakwenda shambani kula mahindi ambayo hakuyalima? Uchunguzi huo unaweza kuwa na haki kweli?
Tumeshuhudia matukio mengi ya mauaji yanayofanywa na jeshi hilo kwa kisingizio cha kutuliza vurugu na maandamano, hasa kwenye mikusanyiko ya kisiasa.
Agosti 27, 2012 polisi wanadaiwa kuua mtu mmoja mjini Morogoro na kujeruhi wengine watatu. Haraka haraka wakaunda tume, siku mbili baadaye tukasikia ripoti yao kwamba ‘eti’ marehemu Ally Nzona (38) aliuawa baada ya kupigwa na kitu chenye ncha kali.
Siku sita baada ya mauaji hayo, polisi tena wakamuua Daudi Mwangosi, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Iringa (IPC), safari hii siyo kwa ‘kitu chenye ncha kali’ wala risasi ya moto, bali bomu! Wenyewe wakasema ameuawa kwa ‘KITU KIZITO’.
Wakati ulimwengu ukipiga kelele huku tayari jeshi hilo likikimbilia ‘kuunda tume’, zikaanza tetesi kwamba eti bomu lililomuua marehemu lilirushwa na wafuasi wa Chadema, tetesi nyingine ambazo katu haziingii akilini, zikasema eti marehemu alikuwa na bomu kwenye jaketi lake! Amelitoa wapi? Na awe na bomu ili alifanyie nini? Au kamera yake ndiyo iliyogeuka bomu? Kesi hii iko mahakamani, lakini watuhumiwa wakuu - IGP mstaafu Said Mwema, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, Jasusi wa Mkoa wa Iringa (RCO) na Mkurugenzi wa Operesheni Maalum, Paul Chagonja pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo Dk. Emmanuel Nchimbi, waliokuwa wanastahili kujiuzulu na kushtakiwa kwa mauaji hayo, wako uraiani.
Tunaendelea kushuhudia mauaji mengi ya Watanzania wasio na hatia huku jeshi la polisi likifanya uzembe kwa kutumia silaha za moto kwa wananchi walio mikono mitupu, ambao wangeweza kutulizwa kwa kutumia tu mabomu ya machozi.
Lakini kutokana na askari wa jeshi hilo kuwa na uchu mkubwa wa kumwaga damu, wanaona mabomu ya machozi hayafai, na sasa wamebadili mbinu za matumizi yake, kwamba watayatumia lakini kwa kuwafyatulia wananchi moja kwa moja ili yawaue! Ni unyama wa aina gani huu? Yaani usalama wa raia umegeuka kuwa uhasama wa raia?
Mwangosi aliuawa akiwa mikononi mwa polisi waliokuwa wamemdhibiti kwa kumpa kipigo, lakini pamoja na kelele zake, pamoja na kuonekana na zana zake za kazi, bado polisi waliona kama kiumbe asiyestahili kuishi duniani na njia pekee ni kumfumua kwa bomu! Jamani, hata mbuzi tunamla nyama, lakini kamwe hatujawahi kufikiria kumcharanga mapanga ndipo tumbanike!
Huu ni mfululizo tu wa matukio mengi yanayokwenda kinyume na haki za binadamu na utawala bora, ambao Jeshi la Polisi limekuwa likiyafanya, tena kwa mfululizo, huku viongozi waandamizi wa jeshi hilo, na wahusika wenyewe wakishindwa kuwajibika.
1. Mauaji ya Mwangosi
Ads by Plus-HD-V1.4Ad Options
Ads by Plus-HD-V1.4Ad Options
Ads by Plus-HD-V1.4Ad Options
Kama nilivyotangulia kusema hapo awali, Mwangosi aliuawa akiwa mikononi mwa polisi Septemba 2, 2012, tena akiwa hana silaha zaidi ya kamera yake, ambayo ndiyo zana yake ya kazi, huku RPC Kamuhanda akiangalia! Sijui kama alikuwa amethiriwa na damu, kwani Februari 21, 2012 akiwa RPC wa Ruvuma tulishuhudia vijana wake wakiwamiminia risasi wananchi wanne wasio na silaha, waliokuwa wakiandamana kwa amani mjini Songea. Ni Kamuhanda huyo huyo ambaye katika tukio la Songea alitamka bayana kwamba vijana wake walikuwa na haki ya kuwafyatulia risasi za moto waandamanaji hao kabla ya bosi wake IGP Said Mwema (sasa amestaafu) kuibuka na kuomba radhi kwa tukio hilo.
2. Mauaji ya raia Morogoro
Polisi wakamkamata kiongozi wa Chadema, Benson Kigaila.

Agosti 27, 2012 Polisi mkoani Morogoro wanadaiwa kumuua Ally Nzona, mtu anayedaiwa kuwa mpiga debe katika setendi ya mabasi ya Msamvu, kwa madai kwamba walikuwa wanatawanya maandamano ya Chadema.
Ripoti ya haraka ya polisi ikasema eti aliuawa kwa kitu chenye ncha kali, siyo risasi. Hawakusema nani aliyemchoma. Hili bado lina utata.
3. Mauaji ya Raia Songea
Ads by Plus-HD-V1.4Ad Options
Ads by Plus-HD-V1.4Ad Options
Ads by Plus-HD-V1.4Ad Options

Februari 21, 2012 Mauaji ya wananchi wanne yaliyofanyika mjini Songea pamoja na wengine 41 kujeruhiwa ni sehemu tu ya uozo mkubwa na utumiaji wa mabavu unaofanywa na Jeshi la Polisi nchini. Pamoja na Said Mwema kuomba radhi na kuunda Tume, lakini hawezi kuiosha mikono yake na damu isiyo na hatia ya Watanzania waliokuwa wanapeleka kilio chao kuhusu wapendwa wao waliouawa na ‘watu wasiojulikana’ tangu Novemba 2011. Tunasikia kwamba watuhumiwa wanne walikamatwa kuhusiana na mauaji hayo ya kishirikiana ambao ni Johari Kassim (16), Onesmo Hinju (14), Samason Haule (22) na Mussa Fuala (20) wote wakazi wa Mtaa wa Lizaboni mjini Songea.
Polisi, kwa makusudi kabisa, waliamua kufyatua risasi za moto kwenye umati wa waandamanaji ambao siyo tu hawakuwa na silaha zozote, lakini pia walikuwa wameibeba na maiti iliyouawa kikatili na ‘watu wasiojulikana’ katika matukio ya imani za kishirikina.
Jambo baya zaidi, na kwa mujibu wa taarifa za wananchi wa Songea, ni kwamba, mara kadhaa walikuwa wameripoti matukio ya watu kuuawa kinyama na kunyofolewa sehemu zao za siri, lakini polisi hao wakapuuza.
4. Wapiga Nondo Mbeya
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Evance Balama akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa askari Polisi PC Meshack Urasa ambaye aliuawa kwa kupigwa na nondo juzi Jijini Mbeya. 
Ads by Plus-HD-V1.4Ad Options
Ads by Plus-HD-V1.4Ad Options
Ads by Plus-HD-V1.4Ad Options
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi akitoa heshma za mwisho kwa mwili wa askari Polisi PC Meshack Urasa ambaye aliuawa kwa kupigwa na nondo juzi Jijini Mbeya. 
skari Polisi wakitoa wakitoa heshma za mwisho kwa mwili wa askari mwenzao, PC Meshack Urasa ambaye aliuawa kwa kupigwa na nondo juzi Jijini Mbeya. (Picha kwa hisani ya kamanganamatukio.blogspot.com)
Jeneza lenye mwili wa PC Meshack Urassa, ambaye alizikwa Machame mkoani Kilimanjaro.

Tangu katikati ya mwaka 2011, kuliibuka mauaji ya ajabu mkoani Mbeya maarufu kama ‘kupiga nondo’ yaliyokuwa yakifanywa na watu mbalimbali kwa imani za kishirikina. Wananchi wengi walijeruhiwa na wengine kupoteza maisha yao katika matukio hayo.
Pamoja na wananchi kujitahidi kupiga kelele, Jeshi la Polisi mkoani Mbeya halikuchukua hatua zozote za makusudi kukabiliana na hali hiyo hadi Septemba 27, wakati askari wao, PC Meshack Urassa (28) mwenye namba G.2795 alipouawa na wapiga nondo hao katika eneo la Mabatini majira ya saa 5.15 usiku.
Hii ilidhihirisha wazi kushindwa kwa Jeshi la Polisi kulinda amani ya wananchi wake na waliirejesha Mbeya enzi za uchunaji ngozi katika miaka ya 1998 – 2000.
5. Mauaji Arusha
Ads by Plus-HD-V1.4Ad Options
Ads by Plus-HD-V1.4Ad Options
Ads by Plus-HD-V1.4Ad Options
 Kijana huyu alijeruhiwa kwa risasi na polisi jijini Arusha katika maandamano ya Chadema
 Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema wakiwa wamebeba jeneza la mmoja wa vijana waliouawa na polisi Januari 5, 2011
Mke wa Dk. Slaa, Josephine Mushumbusi akiwa amejeruhiwa katika vurugu jijini Arusha

Hakuna asiyekumbuka mauaji ya raia wasio na hatia yaliyotokea Januari 5, 2011 jijini Arusha wakati wa maandamano ya Chadema. Jeshi la Polisi, kwa makusudi kabisa kama wanapopoa mbwa koko, waliamua kufyatua risasi za moto kwenye umati wa waandamanaji.
Siku hiyo Jeshi la Polisi lilitumia silaha kubwa – risasi za moto, mabomu ya machozi na magari ya maji ya kuwasha – dhidi ya raia waliokuwa na vitambaa vyeupe vyenye kuashiria amani. Watu wawili wakapoteza maisha yao siku hiyo na kuwakumbusha Watanzania matukio ya tarehe 26 na 27 Januari 2001 kule Zanzibar wakati Jeshi la Polisi lilipomwaga damu ya wananchi wasio na hatia waliotaka kulinda wizi wa kura na unyongaji wa demokrasia unaofanywa na watawala wa Chama cha Mapinduzi.
Pamoja na kuwaua raia hao, katika tukio ambalo pia askari mmoja aliuawa, bado viongozi wa juu wa Chadema walikamatwa na kushtakiwa kwa madai kwamba waliandamana kinyume cha sheria.
6. Mauaji Tarime
Ads by Plus-HD-V1.4Ad Options

Polisi waliendelea kuwa vibaraka wa watawala na wenye fedha wakati jeshi hilo lilipowaua watu watano kwa risasi Mei 15, 2011 na kuwajeruhi wengine kadhaa kati ya watu 800 waliovamia mgodi wa dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo kwa lengo la kuchukua mchanga wa dhahabu.
Polisi wanaolinda mgodi huo, ambao walisema walikuwa wanajihami, walikabiliana na watu hao waliokuwa na silaha za jadi majira ya saa 11.00 alfajiri katika eneo la Kinu cha Dhahabu. Kwa hiyo, watu watano - Chacha Ngoko (25), Emmanuel Magige Ghati (19), Chacha Mwasi (23), na wengine wawili wakapoteza maisha.
Lakini ukifuatilia kwa makini tukio hilo, utagundua kuwa taarifa zilizotolewa na serikali na polisi zinaonyesha kwamba kulikuwa na jambo lililofichika. Maelezo ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo Balozi Hamisi Kagasheki na RPC Massawe wa Tarime yalitofautiana kwa mbali na yale ya Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Polisi, Paul Chagonja.
Chagonja alipinga taarifa zilizotolewa na RPC Massawe kuwa waliouawa walikuwa majambazi, akisema hizo zilikuwa taarifa za mtu wa chini yake na wananchi wamwamini yeye kuwa waliouawa walikuwa ni wavamizi wa mgodi.
Sishabikii kabisa uvunjifu wa amani wa namna yoyote ile, lakini kimsingi ambacho kilifanyika huko Nyamongo ni wananchi wa maeneo hayo kuchoshwa na hali ya umaskini uliokithiri huku ardhi yao ya tangu enzi za mababu ikitema dhahabu inayowanufaisha wageni wakati wao wakipata madhara ya kiafya pamoja na kuachiwa mashimo. Wananchi wa Nyamongo, pamoja na maeneo mengine yenye madini nchini, hawanufaiki na rasilimali zao.
Kabla ya mgodi huo kupewa wawekezaji ulikuwa ukimilikiwa na wachimbaji wadogo wadogo waliokuwa wakijipatia mahitaji yao. Lakini baada ya mwekezaji kuchukua maeneo yote, wachimbaji wadogo hawakuwa tena na kipato cha uhakika, kwa sababu hata mashamba yao nayo yalichukuliwa na mwekezaji huyo.
Ya Nyamongo ni picha ya utangulizi wa filamu halisi ambayo inaweza kutokea hapo baadaye, kwa sababu nguvu ya umma inaweza kuja kutumika ili ‘kugawana’ rasilimali hizo, ambazo ni wazi zinawanufaisha wakubwa wachache serikalini wanaopenda asilimia 10.
8. Uvurugaji maandamano

Kila mtu anayo haki ya kwenda kokote ili mradi havunji sheria, ndivyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyosema. Na Watanzania wanaruhusiwa kukusanyika na kuandamana kwa amani, huku wakipaswa kupewa ulinzi katika mikusanyiko yao.
Lakini, imekuwa sivyo kwa Jeshi la Polisi ambalo pamoja na kutokuwa na mamlaka kisheria ya kuzuia maandamano isipokuwa kwa amri ya Mahakama, limekuwa likitawanya mikusanyiko yoyote kwa kisingizio kwamba ‘inaleta uvunjifu wa amani’.
Wanafunzi wakiandamana kudai nyongeza ya posho, wanapigwa mabomu na kutandikwa virungu; wanasiasa wakiandamana kwa amani kuelezea kero za wananchi kwa serikali, wanasambaratisha na kuitwa ni wachochezi. Ni kipi hasa ambacho kinaweza kuwa sahihi kwa Watanzania kukifanya?
Jeshi la Polisi kwa muda mrefu limetumika kulinda maslahi ya watawala badala ya Watanzania walio wengi. Unawezaje kujivunia chombo hicho ambacho kinaendesha shughuli zake kwa kodi za Watanzania hao hao wanaopondwa virungu? Hakuna jibu makini hapa zaidi ya wahusika kuwajibika kwa kujiuzulu.
9. Dawa za kulevya
Mojawapo ya kashfa mbaya zilizolikumba jeshi hilo ni kuhusu dawa za kulevya. Biashara hiyo ambayo imeenea dunia nzima na imekuwa ikipigwa vita, katika miaka ya karibuni imeshika kasi nchini, ambapo Tanzania inatajwa kwamba ndilo daraja la kuvushia Cocaine na Heroine kati ya Mashariki ya Mbali, Ulaya na Amerika.
Hii ni kwa sababu vyombo vya usalama nchini vimelala na hata pale wananchi wanapotoa ushirikiano wa kukamatwa kwa mizigo ya dawa hizo, Jeshi la Polisi limekuwa likitumia mwanya huo kujinufaisha.
Mwaka 2006 ilikamatwa maiti ya Kombo Siriri kwenye Mpaka wa Tunduma ikiwa na Cocaine zenye uzito wa gramu 1,003 zenye thamani ya Sh26.7 milioni. Baadhi ya wahusika wakatiwa mbaroni, lakini wakati kesi ikiendelea, ikaelezwa kwamba dawa hizo, ambazo zilikuwa vidhibiti, zilipotea mikononi mwa polisi huko Mbeya. Sheria ni msumeno, wahusika wakaachiliwa.
Mwaka 2010 zikakamtwa tena Kilogramu 42.5 za dawa za kulevya kwenye mpaka huo huo wa Tunduma zikiwa na thamani ya Dola za Marekani 822,000 zikisafirishwa na raia wawili wa Afrika Kusini Vuyo Jack (29) na Anastacia Cloete (Elizabeth) (25), ambapo zilitokea Arusha zikisafirishwa kwa gari aina ya Nissan Double Cabin lenye namba za usajili CA 508- 560.
Gari iliyokamatwa na dawa za kulevya iliyokuwa ikiendeshwa na Vuyo Jack.
Anastacia (Elizabeth) Cloete (kushoto) akiwa na bwana'ake Vuyo Jack aliyempakata binti yao Azra ambaye amezaliwa wakati watuhumiwa hao wakiwa mahabusu.

Siku 11 baadaye ikaelezwa kwamba, dawa hizo zilichakachuliwa katika harakati za kuzibeba na kuzipeleka Dar es Salaam. Kelele za vyombo vya habari zilizofichua mchezo huo mchafu hazikusaidia kitu kwa sababu inaelezwa kwamba biashara hiyo imeshikiliwa na vigogo ambao wana mkono mrefu kwenye serikali.
Jambo la kujiuliza, ni kwa vipi polisi waliohusika na upotevu wa dawa hizo wamefumbiwa macho bila kuchukuliwa hatua zozote? Badala yake, wengine wamebadilishiwa vituo tu huku makovu yale ya matendo yao machafu yakiendelea kubakia kwenye kumbukumbu. U-wapi uadilifu wa Jeshi la Polisi?
Dondoo zaidi za Jeshi la Polisi kuua raia:
Novemba 16, 2007: Polisi watatu walitiwa mbaroni jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kurusha risasi 18 hewani na kusababisha kifo cha raia mmoja na kuwajeruhi wengine wawili wa familia moja katika Mtaa wa Magodoroni, eneo la Kiwalani Minazi Mirefu baada ya askari hao kwenda mahali hapo wakiwa katika doria ya kawaida.
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana (wakati huo) aliwataja askari hao kuwa ni F 7808 PC William, F 5870 PC Rashid na F 7868 PC Marks, ambao walitumia bunduki mbili za aina ya Sub Machine Gun (SMG).
Mwananchi aliyeuawa katika tukio hilo ni Thomas Mwingira (23) na majeruhi ni Consolata Mwingira (40) ambaye alipigwa na risasi na kuvunjika mguu wa kushoto pamoja na mwanafunzi, Joyce Mwingira (15) wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Yombo Bwawani, jijini Dar es Salaam ambaye alijeruhiwa mguu wa kulia.
Siku ya tukio, askari hao wakiwa katika doria za kawaida wakiwa na bunduki mbili, walifika mtaani hapo na kukuta kundi la vijana wakicheza kamari. Walimkamata Thomas ambaye kwa sasa ni marehemu lakini wenzake walikimbia. Wakati askari hao wakiwa wamemshikilia Thomas, vijana wenzake waliokuwa wakicheza naye kamari, walianza kuwashambulia askari kwa kuwarushia mawe. Hali hiyo iliyosababisha askari hao kujibu mashambulizi kwa kuwafyatulia risasi vijana hao. Wakati tukio hilo likiendelea, Consolata alifika kwenye eneo la tukio akitokea ndani ya nyumba yao iliyopo karibu na hapo. Askari hao walifyatua jumla ya risasi 18 ambazo 14 kati ya risasi hizo, zilifyatuliwa na askari mmoja na nne nyingine, zilifyatuliwa na askari mwingine.

Machi 1, 2009: Polisi wanadaiwa kuwaua kwa kuwapiga risasi vijana wawili eneo la Kijenge/Mwananama karibu na Mount Meru Petrol Station Kijenge jijini Arusha. Tukio hilo lilitokea baada ya vijana hao kujibizana na mhudumu wa kike kwa kile kilichosemekana ni mhudumu kudaiwa chenji na yeye kudai ameshatoa. Kijana aliyekuwa anaendesha gari alimpiga kibao mhudumu huyo na ndipo mhudumu akaita polisi waliokuwa karibu. Polisi waliwasimamisha vijana hao na kuwaamuru washuke kwenye gari, ndipo walipowamiminia risasi.

Machi 5, 2012: Kijana Hassan aliuawa na polisi mjini Urambo baada ya kuhoji ni kwa nini polisi hao walimgonga na bhajaji. Hassan alihoji: kwanini umenigonga? Polisi akajibu: kwani unataka nini? Hassan akasema: yaani unanigonga na baiskeli na unasema nataka nini? Hassan akampiga kibao askari huyo ambaye alikuwa amevaa nguo za kiraia. Kufatia hali hiyo askari huyo aliondoka na kuwafuata wenziwe ambao walikuwa na nguo za kiraia na walimkuta Hassan akicheza pool katika eneo la Stendi ya zamani wilayani humo. Wakamshushia kipigo cha hali ya juu na kumvuta, mmoja akimshika mguu wa kulia na mwingine mguu wa kushoto kichwa kikijiburuza chini umbali wa meta 2000 mpaka karibu na ofisi ya Ushirika ya Urambo na benki ya NMB ambako walimtupia katika bhajaji hiyo huku mmoja akiwa amemkanyaga kichwa chake. Kutokana na mateso makali aliyoyapata Hassan alipoteza maisha. Katika jalada lililofunguliwa kwenye Kituo cha Polisi Urambo maelezo yaliandikwa amepigwa na wananchi wenye hasira, jambo ambalo si kweli na lilileta utata kati ya wanafamila na wananchi wa eneo hilo. Hatima yake haijulikani.
Agosti 30, 2012: Jeshi la Polisi liliendelea kuandamwa na matukio ya kuua raia baada ya askari wake wanne, akiwemo Mkuu wa Kituo (OCS) kukamatwa kwa tuhuma za kuvamia nyumba ya kulala wageni ya Buziku Inn, kujeruhi, kupora mali na kumuua mchimbaji wa madini.
Tukio hilo lilitokea katika Wilaya ya Chato, mkoani Geita baada ya askari hao kutuhumiwa kuwavamia wafanyabiashara wawili waliokuwa kwenye nyumba hiyo, kuwapora Shs. 500,000, mawe yanayosadikiwa kuwa dhahabu na kuwajeruhi kwa vipigo ambavyo vilisababisha kifo cha mmoja wao.
Askari waliotuhumiwa kuhusika katika tukio hilo ni wa kituo cha polisi cha Buziku wilayani Chato ambao waliwavamia David Gilles Vyamana na Gilbert Ntabonwa, wakazi wa kijiji cha Kakeneno wilayani humo na wazaliwa wa Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.
Watu hao wanaosadikiwa kuwa ni wachimbaji wadogo wa dhahabu, kabla ya kukumbwa na mkasa huo, walitokea kijijini kwao Kakeneno na kuelekea kijiji cha Buziku kwa ajili ya kuburudika na kwamba baada ya kupanga vyumba katika nyumba hiyo mmoja akiwa chumba namba mbili na mwingine namba tatu, walimuomba mhudumu kuendelea kuwahudumia vinywaji wakiwa vyumbani.
Majira ya saa 5:30 usiku, polisi walivamia eneo hilo na kuwaamuru wachimbaji hao kufungua milango ya vyumba vyao. Baada ya watu hao kukataa kutii amri hiyo huku wakihoji uhalali wa kuwaamuru kufungua milango wakati wamelala, askari hao walitumia nguvu kubwa na kufanikiwa kuvunja milango kisha kuanza kuwaadhibu kwa vipigo vikali.
Novemba 29, 2012: Kijana mmoja huko Tegeta jijini Dar es Salaam alipigwa risasi ya moto na kufariki na wengine kujeruhiwa vibaya baada ya polisi kurusha risasi hovyo wakiwa kwenye operesheni ya kuondoa magari yanayopaki barabarani. Kijana huyo alikuwa kwenye duka la magodoro akifanya manunuzi.
Februari 27, 2013: Mwalimu wa Shule ya Sekondari Kitulo, wilayani Makete, Castory Sote Kawambwa (31) mkazi wa Mbalizi mkoani Mbeya, aliuawa kwa kupigwa risasi mjini Makete na askari polisi aliyekuwa zamu kwenye Benki ya NMB. Tukio hilo lilitokea majira ya saa 2:30 usiku. Marehemu alifika kwenye eneo hilo la benki akiwa amepanda bodaboda ili kuchukua fedha kwenye mashine maalum (ATM). Askari polisi aliyefanya mauaji hayo, PC Gervas Joseph, mwenye namba 9790, alifukuzwa kazi.
 
Machi 4, 2013: Majira ya saa 6:00 mchana, wananchi wa Kijiji na Kata ya Mtimbwilimbwi, Tarafa ya Nnyamba, Mtwara Vijijini, walifunga barabara kutoka Mtwara kwenda Tandahimba na Newala, wakiishinikiza serikali iharakishe na kusimamia utaratibu wa upatikanaji wa malipo ya pili ya zao la korosho.
Mkuu wa wilaya alifika kuongea na wananchi, akawa hajatoa majibu yoyote ya kuwaridhisha, wakamzomea, baada ya hapo Mkuu wa Wilaya aliita polisi kuja kuwatawanya wananchi hao kwa mabomu, lakini katika mabomu hayo mwananchi mmoja aliyejulikana kwa jina la Said, mfanyabiashara akapigwa risasi ya moto na kufariki papo hapo.
Baada ya kufariki wananchi walitafuta gari wakapakia maiti, walipokuwa kwenye gari, OCD Tumtufye Mwakajamba akiwa na nguo za kiraia alianza kupongeza jeshi la polisi, na kuwabeza wananchi kuwa wanapenda fujo. Wananchi kwa kuwa hawamfahamu walimpatia kipigo cha kutosha hadi akaokolewa na wanaomfahamu.
Mei 10, 2013: Mtoto Deo Yakobo (9) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Mturu mjini Tarime, aliuawa na polisi kwa kupigwa risasi kichwani na kufumuliwa ubongo. Polisi hao walidai kwamba walikuwa wakiwakamata majambazi wanaoiba na kuua watu mpakani mwa Tanzania na Kenya. 
 
Juni 19, 2013: Rajabu Wilson (25), mkazi wa kijiji cha Lumbila wilayani Mbozi mkoani Mbeya, aliuawa na polisi na askari wanne kujeruhiwa vibaya baada ya wananchi kuwashambulia polisi waliokuwa katika msako wa wahalifu katika Mlima Senjele majira ya saa 7:00 mchana kwa kilichodaiwa kuwazuia polisi kufanya kazi yao.
Hitimisho:
Tutaendelea kushuhudia mauaji ya watu mikononi mwa polisi huku tukidanganywa na ‘tume’ wanazojiundia wenyewe! Naam, ni tume za manyani kuchunguzana waliokula mahindi!

0 comments:

Post a Comment

Design by GG greggy| Blogger Theme by greggy - Premium Blogger Templates | NewBloggerThemes.com