Friday 19 December 2014


Pichani ni Bosi wa IPTL Bwana  Harbinder Singh Sethi
NA KAROLI VINSENT
RAIS  Jakaya Kikwete amehailisha Mkutano wake kati ya Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam  uliokuwa ufanyike leo Katika Ukumbi wa Ubungo plaza mpaka Jumatatu ya Wiki Ijayo.
    Sababu ya Kuhailisha Mkutano huo bado haijasemwa ila Wadadisi wa masuala ya Mambo wanasema Sababu ya Rais Jakaya Kikwete Kuhailisha Mkutano huo inatokana na  Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na wenzake wawili, kufungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakiiomba  itoe amri ya kuzuia utekelezaji wa maazimio nane ya Bunge kuhusu kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).



 Mbali na hao,Wengine waliofungua kesi hiyo namba 59 ya mwaka 2014, ni kampuni ya Pan Power Solution Tanzania (PAP) na mmiliki wake, Harbinder Singh Sethi.IPTL, PAP na Sethi walifungua kesi hiyo jana chini ya hati ya dharura kupitia kampuni za mawakili ya Bulwark, Asyla na Marando and Mnyele.

          Wadaiwa katika kesi hiyo ni Waziri Mkuu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

               Katika hati ya madai iliyowasilishwa katika mahakama hiyo jana, wadai wanapinga maazimio ya Bunge kutekelezwa wakidai kwamba, kilichofanyika bungeni ni kinyume cha katiba ya nchi.

           Wanadai maazimio hayo yanalenga kugombanisha mihimili mitatu ya dola na kwamba, yaliegemea upande mmoja.Pia wanadai kwamba, kuna kesi mbalimbali zinazoendelea mahakamani zinazohusiana na sakata la fedha hizo.

           Vilevile, wanadai Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alifanya ukaguzi, pia Takukuru ilifanya uchunguzi, hatimaye taarifa ya CAG ikajadiliwa bungeni.
 Wanadai kwamba mjadala huo ulisababisha Bunge kufikia maazimio hayo.

          Wadai hao wanadai kitendo hicho kilipuuza amri ya Mahakama Kuu kwa kufuata tafsiri potofu iliyotolewa na Waziri wa Katiba na Sheria kuhusu amri iliyozuia mjadala wa akaunti hiyo kufanyika bungeni.

          Kutokana na sababu hizo, wanaiomba mahakama izuie utekelezwaji wa maazimio ya Bunge.Pia itangaze maazimio hayo yaliyofikiwa Novemba 29, mwaka huu na maamuzi ya Spika wa Bunge kuyakubali, kuwa ni kinyume cha katiba ya nchi.

        Kesi hiyo iliyofunguliwa leo mchana, inatarajiwa kuanza kusikilizwa mara tu baada ya jopo la majaji watakapoteuliwa.

MAAZIMIO YA BUNGE
Azimio la kwanza lililofikiwa na Bunge linataka Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua stahiki za kisheria watu wote waliotajwa na taarifa maalumu ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (CAG) kuhusika na kashfa hiyo na watu wengine watakaogundulika kuhusika kufuatia uchunguzi mbali mbali unaoendelea.

La pili linataka Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhingo; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka; aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema; Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wawajibishwe, kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao.

Wengine waliotajwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusika katika kashfa hiyo ni Sethi na mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing, James Rugemalira.

Azimio la tatu linataka kamati za kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka kabla ya mkutano wa 18 wa Bunge, kuwavua nyadhifa wenyeviti wa kamati za Bunge; Andrew Chenge (Bajeti), Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini) na William Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala).

La nne linataka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Azimio la tano linataka mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Benki ya Stanbic Bank (Tanzania) Ltd na benki nyingine yoyote itakayogundulika kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika akaunti hiyo, kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.

 La sita linataka serikali iandae na kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria iliyoiunda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Azimio la saba linataka serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha za shirika hilo.

Na azimio la nane linataka serikali itekeleze azimio husika la Bunge mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti na serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme.

0 comments:

Post a Comment

Design by GG greggy| Blogger Theme by greggy - Premium Blogger Templates | NewBloggerThemes.com