Thursday 18 December 2014


Aisha Madinda akiwa na mkurugenzi wa ASET Asha Baraka.
Makala: Sifael Paul na Gladness Mallya
Amekwenda mapema mno! Siku ya Desemba 17, mwaka huu haikuwa poa hata kidogo kwenye tasnia ya muziki wa dansi Bongo katika kipengele cha unenguaji.
Chumba chetu cha habari cha Global Publishers kinachofanya kazi kwa karibu na mastaa Bongo kilipata mshtuko wa aina yake.
Zilikuwa ni habari mbaya za kifo cha aliyekuwa mnenguaji bei mbaya wa Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’ inayosimamiwa na Kampuni ya ASET chini ya mkurugenzi wake, Asha Baraka, Mwanaisha Mohamed Mbegu. Wengi tulimzoea kwa jina la stejini la Aisha Madinda.
AZALIWA OCEAN ROAD
Katika mahojiano aliyofanya na magazeti yetu kwa nyakati tofauti, kabla ya kujiingiza kwenye sanaa ya unenguaji na baada ya kuugua kwa muda mrefu kisha kupona na kukutwa na umauti, Aisha alieleza kwamba alizaliwa jijini Dar katika Hospitali ya Ocean Road.
KIGOMA
Hiyo ilikuwa Mei 5, 1979. Hivyo ameondoka mapema akiwa na umri wa miaka 35 tu. Baada ya maisha ya utoto, Aisha alipelekwa mkoani Kigoma ambako ndiko alikokulia.
Akiwa mkoani humo, Aisha alipata masomo yake ya msingi katika Shule ya Kiganamo iliyopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma hadi alipohitimu darasa la saba mwaka 1992.
AISHIA FORM TWO
Mwaka 1993 alihamishia makazi yake mjini Kigoma na kujiunga na Sekondari ya Katubuka. Hata hivyo, Aisha hakufanikiwa kuhitimu masomo yake ya sekondari baada ya wazazi wake kushindwa kumlipia ada hivyo aliishia kidato cha pili (form two).
DAR
Mwaka 1994, Aisha alihamia jijini Dar na kuanza kazi ya usafi katika kampuni iliyojulikana kama Dar Cleaner. Alifanya kazi hiyo katika majengo mbalimbali ya jijini hivyo kufahamiana na watu wengi.
UNENGUAJI
Mwaka 1996 aliingia kwenye unenguaji baada ya prodyuza wa muziki aliyefahamika kwa jina moja la Maloni kumtonya kuwa Club Bilicanas ‘Bilz’ iliyopo Posta, Dar kulikuwa kunahitajika wanenguaji.
Akiwa Bilz, mwaka huohuo, klabu hiyo ilianzisha bendi iliyokwenda kwa jina la Bil Bams ndipo Aisha akaanza kuitumikia.
UARABUNI
Mwaka 1999, wakati huo, Aisha alishakuwa tishio katika kukata nyonga stejini huku akieleza jinsi alivyoipenda kazi yake hiyo.
Mwaka huohuo, alipata shavu la kwenda kupiga kazi Uarabuni katika Mji wa Muscat akiwa ameambatana na mcheza shoo mwenzake, Halima White ambaye sasa ni marehemu.
Walikaa nchini humo kwa takriban mwaka mmoja, mwaka 2000 walirejea Bongo wakiwa mambo safi.
BORABORA SOUND
Mwaka huo Aisha alijiunga na Bendi ya Borabora Sound ambayo aliitumikia kwa miezi sita kabla ya kusafiri tena kwenda Bahrain, Uarabuni kwa kazi hiyo ya unenguaji.
KILIMANJARO CONNECTION
Baadaye Aisha alirejea Dar kwa mara nyingine. Alijiunga na Bendi ya Kilimanjaro Connection ya jijini Dar ambapo pia hakukaa sana.
Mwaka 2000 mwishoni, aliachana na bendi hiyo kisha akawa anafanya biashara zake ndogondogo.
Aisha Madinda.
TWANGA PEPETA
Mwaka 2001, mkali huyo wa kukata nyonga anayeshikilia rekodi hiyo kwa kipindi chote alijiunga na Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’.
UHOLANZI
Aisha alifanya safari nyingi za kisanaa barani Ulaya akiwa na Twanga Pepeta lakini hawezi kusahau shoo aliyokwenda kufanya nchini Uholanzi katika Mji wa Amsterdam ambako alipokelewa kwa shangwe ya ajabu kiasi kwamba hakuamini macho yake.
EXTRA BONGO
Hapo alipiga kazi ya unenguaji hadi mwaka 2011 mwishoni alipohamia Bendi ya Extra Bongo ‘Wazee wa Kizigo Staili’.
Kwa bahati mbaya, wakati huo Aisha tayari alikuwa ameshatopea kwenye matumizi ya madawa ya kulevya hadi kufikia hatua ya kushindwa kunengua akisumbuliwa na tatizo la kuvimba miguu. Hata hivyo, alitangaza kuacha kutumia madawa hayo japokuwa baadaye kuliibuka ‘rumansi’ kuwa bado alikuwa akitumia.
REJEA TWANGA
Mwaka jana, mwanamama huyo alirejea Twanga Pepeta lakini bado alikuwa akisumbuliwa na miguu huku akitumia dozi ya kuacha madawa ya kulevya na kuhamasisha vijana kuacha ulevi huo mbaya unaomaliza nguvu ya taifa ambayo ni vijana.
OKOKA
Katika kutafuta msaada wa kiroho, Aisha aliokoka akawa anasali katika Kanisa la Zoe lililopo Segerea jijini Dar akiyakabidhi maisha yake kwa Mwenyezi Mungu hadi alipokutwa na umauti.
DUBAI
Hata hivyo, miezi kadhaa mwaka huu, mwanadada huyo alitimkia Dubai kwa ajili ya dili la kunengua lakini alipofika huko alijikuta akitumikishwa kazi za ndani na wenyeji wake kiasi cha ubalozi wa Tanzania huko Dubai kuingilia kati na kumrejesha nyumbani.

0 comments:

Post a Comment

Design by GG greggy| Blogger Theme by greggy - Premium Blogger Templates | NewBloggerThemes.com